4 Kwa maana mkifanya haya kweli kweli, ndipo watakapoingia kwa malango ya nyumba hii wafalme wenye kuketi katika kiti cha enzi cha Daudi, wanakwenda kwa magari, na wamepanda farasi yeye, na watumishi wake, na watu wake.
5 Lakini kama hamtaki kusikia maneno haya, mimi naapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, ya kuwa nyumba hii itakuwa ukiwa.
6 Kwa maana BWANA asema hivi, katika habari ya nyumba ya mfalme wa Yuda;Wewe u Gileadi kwangu,na kichwa cha Lebanoni;Ila hakika nitakufanya kuwa jangwa,na miji isiyokaliwa na watu.
7 Nami nitakufanyia tayari watu wenye kuharibu,kila mtu na silaha zake;Nao watakata mierezi miteule yako,na kuitupa motoni.
8 Na mataifa mengi watapita karibu na mji huu, nao watasema kila mtu na jirani yake, Nini maana yake BWANA kuutenda hivi mji huu mkubwa?
9 Ndipo watakapojibu, Ni kwa sababu waliliacha agano la BWANA, Mungu wao, wakaabudu miungu mingine, na kuitumikia.
10 Msimlilie aliyekufa, wala msimwombolezee,Bali mlilieni huyo aendaye zake mbali;Kwa maana yeye hatarudi tena,Wala hataiona nchi aliyozaliwa.