3 kisha uvipeleke kwa mfalme wa Edomu, na mfalme wa Moabu, na mfalme wa wana wa Amoni, na mfalme wa Tiro, na mfalme wa Sidoni, kwa mikono ya wajumbe watakaofika Yerusalemu kwa Sedekia, mfalme wa Yuda.
4 Uwaagize waende kwa bwana zao, na kuwaambia, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mtawaambia bwana zenu maneno haya;
5 Mimi nimeiumba dunia hii, wanadamu na wanyama walio juu ya uso wa nchi, kwa uweza wangu mkuu, na kwa mkono wangu ulionyoshwa; nami nawapa watu kama inipendezavyo.
6 Na sasa nimetia nchi hizi zote katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu; na wanyama wa mwituni pia nimempa wamtumikie.
7 Na mataifa yote watamtumikia yeye, na mwanawe, na mwana wa mwanawe, hata utakapowadia wakati wa nchi yake mwenyewe, ndipo mataifa mengi na wafalme wakuu watamtumikisha yeye.
8 Na itakuwa, taifa lile na mfalme yule asiyetaka kumtumikia Nebukadreza, huyo mfalme wa Babeli, na kutia shingo zao katika nira ya mfalme wa Babeli, mimi nitaliadhibu taifa lile kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, asema BWANA, hata nitakapokuwa nimewaangamiza kwa mkono wake.
9 Lakini, katika habari zenu, msisikilize manabii wenu, wala wabashiri wenu, wala ndoto zenu, wala watambuzi wenu, wala waganga wenu, wanaowaambia, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli;