3 Kwa maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga, akisema, Kwa nini unatabiri, na kusema, BWANA asema hivi, Angalia, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atautwaa;
4 tena, Sedekia, mfalme wa Yuda, hatapona kutoka katika mikono ya Wakaldayo, lakini hakika yake atatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, atanena naye mdomo kwa mdomo, na macho yake yatatazama macho yake;
5 naye atamchukua Sedekia mpaka Babeli, naye atakuwako huko hata nitakapomjilia, asema BWANA; mjapopigana na Wakaldayo hamtafanikiwa.
6 Yeremia akasema, Neno la BWANA limenijia, kusema,
7 Tazama, Hanameli, mwana wa Shalumu, mjomba wako, atakujia, akisema, Jinunulie shamba langu lililoko Anathothi; maana haki ya ukombozi ni yako, ulinunue.
8 Basi Hanameli, mwana wa mjomba wangu, akanijia ndani ya uwanda wa walinzi, sawasawa na lile neno la BWANA, akaniambia, Tafadhali, ulinunue shamba langu lililoko Anathothi, katika nchi ya Benyamini; maana haki ya urithi ni yako, na haki ya ukombozi ni yako; ujinunulie. Ndipo nikajua kama neno hili ni neno la BWANA.
9 Basi nikalinunua shamba lile lililoko Anathothi kwa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, nikampimia fedha yake, shekeli kumi na saba za fedha.