1 Tena, neno la BWANA likamjia Yeremia mara ya pili, hapo alipokuwa akali amefungwa katika uwanda wa walinzi, kusema,
2 BWANA alitendaye jambo hili, BWANA aliumbaye ili alithibitishe; BWANA ndilo jina lake; asema hivi,
3 Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.
4 Maana BWANA, Mungu wa Israeli asema hivi, katika habari za nyumba za mji huu, na katika habari za nyumba za wafalme wa Yuda, zilizobomolewa ili kuyapinga maboma na upanga;
5 Wanakuja kupigana na Wakaldayo, lakini ni kuzijaza kwa mizoga ya watu, niliowaua katika hasira yangu na ghadhabu yangu, ambao kwa ajili ya uovu wao wote nimeuficha mji huu uso wangu.
6 Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli.