28 Kwa hiyo tulisema, Itakuwa, hapo watakapotuambia neno kama hilo, au kuwaambia watu wa vizazi vyetu katika zamani zijazo neno kama hilo, ndipo sisi tutawaambia, Angalieni huu mfano wa madhabahu ya BWANA, walioufanya baba zetu, si kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wala kwa ajili ya dhabihu; lakini ni ushahidi kati ya sisi na ninyi.
29 Mungu na atuzuie msimwasi BWANA, na kukengeuka hivi leo na kuacha kumwandama BWANA, hata mkajenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, au sadaka za unga, au dhabihu, mbali na ile madhabahu ya BWANA, Mungu wetu, iliyo huko mbele ya maskani yake.
30 Basi Finehasi kuhani, na wakuu wa mkutano, maana, ni hao waliokuwa vichwa vya maelfu ya Israeli waliokuwa pamoja naye, hapo walipoyasikia hayo maneno waliyoyasema hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, maneno hayo yaliwaridhia sana.
31 Naye Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, akawaambia wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, akasema, Siku hii ya leo twajua ya kwamba BWANA yu kati yetu, kwa sababu hamkukosa katika jambo hili mbele ya BWANA; sasa ninyi mmewaokoa wana wa Israeli na mkono wa BWANA.
32 Kisha Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, na hao wakuu, wakarudi na kuwaacha wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakatoka katika nchi ya Gileadi, na kuingia nchi ya Kanaani; wakawarudia wana wa Israeli, wakawapa habari.
33 Wana wa Israeli nao wakaliridhia jambo hilo; nao wana wa Israeli wakamhimidi Mungu, wala hawakusema tena habari ya kuwaendea juu yao kupigana nao, wala kuiharibu nchi waliyoikaa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi.
34 Basi hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakaiita madhabahu hiyo Edi; wakasema, Kwa kuwa ni ushahidi kati yetu ya kwamba yeye BWANA ndiye Mungu.