26 Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu pa BWANA.
27 Yoshua akawaambia watu wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno yote ya BWANA aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana Mungu wenu.
28 Basi Yoshua akawaruhusu watu, wakaenda zao, kila mtu kwenye urithi wake.
29 Ikawa, baada ya hayo, Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, mwenye umri wa miaka mia na kumi.
30 Wakamzika katika mpaka wa urithi wake, huko Timnath-sera; ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi.
31 Nao Israeli wakamtumikia BWANA siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya BWANA, aliyowatendea Israeli.
32 Na hiyo mifupa ya Yusufu, ambayo wana wa Israeli walikuwa wameileta kutoka Misri, wakaizika huko Shekemu katika ile sehemu ya nchi, Yakobo aliyoinunua kwa wana wa Hamori, babaye Shekemu, kwa vipande mia vya fedha; nayo ikawa ni urithi wa wana wa Yusufu.