1 Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao wakatoka Shitimu, wakafika mto wa Yordani, yeye na wana wa Israeli wote, wakakaa hapo kabla ya kuvuka.
2 Ikawa baada ya siku tatu, maakida wakapita katikati ya marago,
3 wakawaamuru watu wote wakisema, Mtakapoliona sanduku la agano la BWANA, Mungu wenu, na makuhani Walawi wakilichukua, ndipo mtakapoondoka hapa mlipo na kulifuata.
4 Lakini, na iwe nafasi kati ya ninyi na lile sanduku, kama dhiraa elfu mbili kiasi chake; msilikaribie mpate kuijua njia ambayo hamna budi kuiendea; kwa maana hamjapita njia hii bado.
5 Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho BWANA atatenda mambo ya ajabu kati yenu.
6 Kisha Yoshua akawaambia makuhani, akasema, Liinueni sanduku la agano, mkavuke mbele ya hao watu. Wakaliinua sanduku la agano, wakatangulia mbele ya watu.