16 Basi Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, akawasogeza Israeli kabila kwa kabila; kabila ya Yuda ikatwaliwa.
17 Akazisogeza jamaa za Yuda, akaitwaa jamaa ya Wazera; akaisogeza jamaa ya Wazera mtu kwa mtu; Zabdi akatwaliwa.
18 Akawasogeza watu wa nyumba yake mmoja mmoja; na Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda akatwaliwa.
19 Yoshua akamwambia Akani, Mwanangu, nakusihi, umtukuze BWANA, Mungu wa Israeli, ukaungame kwake; uniambie sasa ulilolitenda; usinifiche.
20 Akani akamjibu Yoshua, akasema, Kweli nimefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wa Israeli, nami nimefanya mambo haya na haya.
21 Nilipoona katika nyara joho nzuri ya Babeli, na shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu, uzani wake shekeli hamsini, basi nalivitamani nikavitwaa; tazama, vimefichwa mchangani katikati ya hema yangu, na ile fedha chini yake.
22 Basi Yoshua akatuma wajumbe wakapiga mbio mpaka hemani; na tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, na ile fedha chini yake.