16 Watu wote waliokuwa ndani ya mji waliitwa wakusanyike pamoja ili kuwafuatia; nao wakamfuatia Yoshua, wakasongea mbele na kuuacha mji.
17 Hakusalia mtu ye yote ndani ya Ai, au katika Betheli, asiyetoka nje kuwafuatia Israeli; wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.
18 Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji.
19 Wale watu waliovizia wakainuka kwa upesi kutoka mahali pao, nao wakapiga mbio mara hapo alipokuwa amekwisha unyosha mkono wake, wakaingia ndani ya mji, na kuushika; nao wakafanya haraka kuuteketeza kwa moto huo mji.
20 Kisha hapo hao watu wa Ai walipotazama nyuma yao, wakaona, na tazama, moshi wa huo mji ulikuwa unapaa juu kwenda mawinguni, nao hawakuwa na nguvu za kukimbia huku wala huku; na wale watu waliokuwa wamekimbia kuenenda nyikani wakageuka na kuwarudia hao waliokuwa wakiwafuatia.
21 Basi hapo Yoshua na Israeli wote walipoona ya kwamba hao waliovizia wamekwisha kuushika huo mji, na ya kwamba moshi wa mji umepaa juu, ndipo wakageuka tena, na kuwaua watu wa Ai.
22 Tena hao; wengine wakatoka nje kuutoka huo mji kinyume chao; basi hivyo walikuwa wa katikati ya Israeli, wengine upande huu na wengine upande huu; nao wakawapiga, hata wasimwache hata mmoja miongoni mwao aliyesalia, wala kupona.