1 Katika mwezi wa nane, mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema,
2 BWANA amewakasirikia sana baba zenu.
3 Basi, uwaambie, BWANA wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema BWANA wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi.
4 Msiwe ninyi kama baba zenu, ambao manabii wa zamani waliwalilia, wakisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Rudini sasa, na kuziacha njia zenu mbovu, na matendo yenu maovu; lakini hawakusikia, wala kunisikiliza, asema BWANA.