2 Angalia, mimi nitafanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumba-yumba kwa watu wa kabila zote, wazungukao pande zote; tena kitakuwa juu ya Yuda pia wakati wa kuhusuriwa Yerusalemu.
3 Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake.
4 Katika siku hiyo, asema BWANA, nitamtia kila farasi ushangao, na yeye ampandaye nitamtia wazimu; nami nitaifunulia nyumba ya Yuda macho yangu, nami nitamtia upofu kila farasi wa hizo kabila za watu.
5 Na wakuu wa Yuda watasema mioyoni mwao, Wenyeji wa Yerusalemu ni nguvu zangu katika BWANA wa majeshi, Mungu wao.
6 Siku hiyo nitawafanya wakuu wa Yuda kuwa kama kigae chenye moto katika kuni, na kama kinga cha moto katika miganda; nao watateketeza watu wa kila kabila, wawazungukao pande zote, upande wa mkono wa kuume na upande wa mkono wa kushoto; na baada ya haya Yerusalemu utakaa mahali pake, naam, hapo Yerusalemu.
7 Naye BWANA ataziokoa hema za Yuda kwanza, ili utukufu wa nyumba ya Daudi, na utukufu wa wenyeji wa Yerusalemu, usipate kutukuzwa kuliko Yuda.
8 Katika siku hiyo BWANA atawalinda wenyeji wa Yerusalemu; na yeye aliye dhaifu miongoni mwao atakuwa kama Daudi siku hiyo; nayo nyumba ya Daudi itakuwa kama Mungu, kama malaika wa BWANA mbele yao.