7 lakini itakuwa siku moja, iliyojulikana na BWANA; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, ya kwamba wakati wa jioni kutakuwako nuru.
8 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba maji yaliyo hai yatatoka katika Yerusalemu; nusu yake itakwenda upande wa bahari ya mashariki, na nusu yake upande wa bahari ya magharibi; wakati wa hari na wakati wa baridi itakuwa hivi.
9 Naye BWANA atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo BWANA atakuwa mmoja, na jina lake moja.
10 Nchi yote itageuzwa kuwa kama Araba, toka Geba mpaka Rimoni upande wa kusini wa Yerusalemu; naye atainuliwa juu, atakaa mahali pake mwenyewe, toka lango la Benyamini mpaka mahali pa lango la kwanza, mpaka lango la pembeni; tena toka mnara wa Hananeli mpaka mashinikizo ya mfalme.
11 Na watu watakaa ndani yake, wala hakutakuwako laana tena; lakini Yerusalemu utakaa salama.
12 Na hii ndiyo tauni, ambayo BWANA atawapiga watu wote waliofanya vita juu ya Yerusalemu; nyama ya mwili wao itaharibika, wasimamapo juu ya miguu yao, na macho yao yataharibika ndani ya vichwa vyao, na ndimi zao zitaharibika vinywani mwao.
13 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba mashaka makubwa yatokayo kwa BWANA yatakuwa kati yao; na kila mmoja wao atakamata mkono wa jirani yake, na mkono wake utainuliwa ili kushindana na mkono wa jirani yake.