28 Alipomwona Yesu, alijitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kubwa, “We, Yesu Mwana wa Mungu Mkuu, una shauri gani nami? Ninakusihi usinitese!”
29 Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia huyo pepo mchafu amtoke mtu huyo. Pepo huyo mchafu alikuwa anamvamia mtu huyo mara nyingi, na ingawa watu walimweka ndani na kumfunga kwa minyororo na pingu, lakini kila mara alivivunja vifungo hivyo, akakimbizwa na pepo huyo mchafu hadi jangwani.
30 Basi, Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?” Yeye akajibu, “Jina langu ni ‘Jeshi’” – kwa sababu pepo wengi walikuwa wamempagaa.
31 Hao pepo wakamsihi asiwapeleke kwenye shimo kuu.
32 Mahali hapo kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha mlimani. Basi, hao pepo wakamsihi awaruhusu wawaingie. Naye Yesu akawapa ruhusa.
33 Kwa hiyo pepo hao wakamtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nao wakaporomoka kwenye ule mteremko mkali, wakatumbukia ziwani, wakafa maji.
34 Wale wachungaji walipoona yote yaliyotokea walikimbia, wakaenda kuwapa watu habari mjini na mashambani.