12 Yesu aliwasikia, akasema, “Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa.
13 Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma, wala si tambiko.’ Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi.”
14 Kisha wanafunzi wa Yohane Mbatizaji walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Sisi na Mafarisayo hufunga mara nyingi; mbona wanafunzi wako hawafungi?”
15 Yesu akawajibu, “Je, walioalikwa harusini hutakiwa kuomboleza wakati bwana arusi yupo pamoja nao? La, hasha! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.
16 “Watu hawatii kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu. Maana kiraka hicho kitararua hilo vazi kuukuu, na pale palipokuwa pameraruka pataongezeka.
17 Wala watu hawaweki divai mpya katika viriba vikuukuu. Wakifanya hivyo, viriba hupasuka na divai ikamwagika, navyo viriba vikaharibika. Ila, watu huweka divai mpya katika viriba vipya, na vyote viwili, viriba na divai, vikahifadhiwa salama.”
18 Yesu alipokuwa akisema hayo, ofisa mmoja Myahudi alifika, akamwinamia na kusema, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini, tafadhali twende umwekee mkono wako naye ataishi.”