12 Kisha, malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ikawekwa kwa ajili ya wafalme kutoka mashariki.
13 Kisha, nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama na kinywani mwa yule nabii wa uongo.
14 Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita ya ile siku kubwa ya Mungu Mwenye Nguvu.
15 “Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo zake ili asije akaenda uchi huko na huko na kuaibika hadharani.”
16 Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa Kiebrania Harmagedoni.
17 Kisha, malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti kubwa ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, hekaluni, ikisema, “Imetendeka!”
18 Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu.