5 Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo “Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani.”
6 Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu.Nilipomwona nilishangaa mno.
7 Lakini malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana vichwa saba na pembe kumi.
8 Huyo mnyama uliyemwona, alikuwa hai hapo awali lakini sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uhai tangu mwanzo wa ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali aliishi, kisha akafa na sasa anatokea tena!
9 “Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme saba.
10 Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia, mmoja anatawala bado na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki kwa muda mfupi.
11 Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini sasa haishi tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na anakwenda zake kuharibiwa.