16 wakisema, “Ole! Ole kwa mji huu mkuu. Ulizoea kuvalia nguo za kitani, za rangi ya zambarau na nyekundu, na kujipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu!
17 Kwa saa moja tu utajiri wako umetoweka!”Halafu manahodha wote na wasafiri wao, wanamaji na wote wanaofanya kazi baharini, walisimama kwa mbali,
18 na walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti: “Hakujapata kuwako mji kama mji huu mkuu!”
19 Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na kuomboleza: “Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli zisafirizo baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa saa moja tu umepoteza kila kitu!
20 “Furahi ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa Mungu, mitume na manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo uliyowatenda nyinyi!”
21 Kisha, malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe mfano wa jiwe kubwa la kusagia, akalitupa baharini akisema, “Ndivyo Babuloni atakavyotupwa na kupotea kabisa.
22 Sauti za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta hazitasikika tena ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile atakayepatikana tena ndani yako; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikika tena ndani yako.