5 “Mshindi atavikwa hivyo kwa mavazi meupe. Nami sitalifuta jina lake kutoka katika kitabu cha uhai; tena nitamkiri kwamba ni wangu mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika wake.
6 “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!
7 “Kwa malaika wa kanisa la Filadelfia andika hivi:“Mimi niliye mtakatifu na wa kweli, ambaye nina ule ufunguo wa Daudi na ambaye hufungua na hakuna awezaye kufunga, hufunga na hakuna awezaye kufungua.
8 Nayajua mambo yako yote! Sasa, nimefungua mbele yako mlango ambao hakuna mtu awezaye kuufunga; najua kwamba ingawa huna nguvu sana, hata hivyo, umelitii neno langu wala hukulikana jina langu.
9 Sikiliza! Nitawapeleka kwako watu wa kundi lake Shetani, watu ambao hujisema kuwa ni Wayahudi, kumbe sivyo, ila wanasema uongo. Naam, nitawapeleka kwako na kuwafanya wapige magoti mbele yako, wapate kujua kwamba nimekupenda wewe.
10 Kwa kuwa wewe umezingatia neno langu la kuwa na uvumilivu thabiti, mimi nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia ulimwengu mzima, kuwajaribu wote wanaoishi duniani.
11 Naja kwako upesi! Shikilia kwa nguvu ulicho nacho sasa, ili usije ukanyang'anywa na mtu yeyote taji yako.