1 Kisha, nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri saba. Nikasikia mmoja wa wale viumbe hai wanne akisema kwa sauti kama ya ngurumo, “Njoo!”
2 Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na mpandafarasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka kama mshindi, aendelee kushinda.
3 Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe hai wa pili akisema, “Njoo!”
4 Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo, mwekundu. Mpandafarasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani duniani, watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa.
5 Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe hai wa tatu akisema, “Njoo!” Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mmoja hapo, mweusi. Mpandafarasi wake alikuwa na vipimo viwili vya kupimia uzito mkononi mwake.