1 Kila kuhani mkuu ambaye huchaguliwa miongoni mwa watu hupewa jukumu la kushughulikia mambo ya Mungu kwa niaba ya watu, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi.
2 Maadamu yeye mwenyewe ni dhaifu, anaweza kuwatendea kwa huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa.
3 Kwa sababu hiyo anapaswa kutoa tambiko si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.
4 Hakuna mtu awezaye kujifanya mwenyewe kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni.
5 Hali kadhalika naye Kristo; yeye hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimteua na kumwambia:“Wewe ni Mwanangu;mimi leo nimekuwa baba yako.”
6 Alisema pia mahali pengine:“Wewe ni kuhani milele,kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.”
7 Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kifoni; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu.