2 Simoni Petro, Thoma (aitwaye Pacha), na Nathanaeli mwenyeji wa Kana Galilaya, wana wawili wa Zebedayo na wanafunzi wake wengine wawili, walikuwa wote pamoja.
3 Simoni Petro aliwaambia, “Nakwenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Nasi tutafuatana nawe.” Basi, wakaenda, wakapanda mashua, lakini usiku huo hawakupata chochote.
4 Kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya ziwa, lakini wanafunzi hawakujua kwamba alikuwa ni yeye.
5 Basi, Yesu akawauliza, “Vijana, hamjapata samaki wowote sio?” Wao wakamjibu, “La! Hatujapata kitu.”
6 Yesu akawaambia, “Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki.” Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki.
7 Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, “Ni Bwana!” Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini.
8 Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia kutoka ukingoni.