8 Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, “Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?”
9 Baadhi yao wakasema, “Ndiye.” Wengine wakasema, “La! Ila anafanana naye.” Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, “Ni mimi!”
10 Basi, wakamwuliza, “Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?”
11 Naye akawajibu, “Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: ‘Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.’ Hapo, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona.”
12 Wakamwuliza, “Yeye yuko wapi?” Naye akawajibu, “Mimi sijui!”
13 Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo.
14 Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato.