17 Daudi akasema kwa hamu kubwa, “Laiti kama mtu angeweza kunipa maji ya kunywa kutoka katika kisima cha Bethlehemu kilicho karibu na lango la mji!”
18 Wale mashujaa wake watatu walitoka, wakapenya katikati ya kambi ya jeshi la Wafilisti, wakaenda na kuchota maji katika kisima cha Bethlehemu, karibu na lango la mji, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa, na badala yake akayamwaga chini kama tambiko kwa Mwenyezi-Mungu
19 akisema, “Tendo kama hili lipitishie mbali nami; siwezi kulifanya mbele ya Mungu wangu. Je, waweza kunywa damu ya maisha ya watu hawa? Maana kwa kuyahatarisha maisha yao walileta maji haya.” Kwa hiyo Daudi hakuyanywa maji hayo. Hayo ndio mambo waliyotenda wale mashujaa watatu.
20 Abishai, nduguye Yoabu, alikuwa mkuu wa mashujaa thelathini. Yeye alipigana kwa mkuki wake dhidi ya watu 300, akawaua, akajipatia jina miongoni mwa wale mashujaa watatu.
21 Basi, akawa mashuhuri zaidi miongoni mwa mashujaa thelathini, hata akawa kamanda wao, lakini hakuwa shujaa kama wale mashujaa watatu.
22 Naye Benaya, mwana wa Yehoyada, kutoka Kabzeeli, alikuwa askari shujaa ambaye alifanya mambo mengi ya ajabu. Aliwaua mashujaa wawili kutoka Moabu, na siku moja wakati wa barafu, alishuka na kuua simba shimoni.
23 Vilevile, alimuua Mmisri mmoja, mtu mrefu sana, urefu wake kama mita mbili, naye mkononi mwake alikuwa amebeba mkuki mkubwa sana, kama mti wa mfumaji. Lakini Benaya alimwendea akiwa na fimbo tu, akamnyanganya mkuki huo, na kumuua Mmisri huyo kwa mkuki wake mwenyewe.