12 wa nane Yohanani, wa tisa Elsabadi,
13 wa kumi Yeremia, na wa kumi na moja Makbanai.
14 Wagadi hao, walikuwa maofisa wa jeshi. Kulingana na vyeo vyao, mdogo alisimamia kikosi cha wanajeshi 100, na mkubwa alisimamia kikosi cha wanajeshi 1,000.
15 Hawa ndio watu waliovuka mto Yordani mnamo mwezi wa kwanza, mto ulipokuwa umefurika pande zote na kuwatawanya watu mashariki na magharibi ya mto.
16 Baadhi ya watu kutoka makabila ya Benyamini na Yuda walifika ngomeni alipokuwa Daudi.
17 Daudi akatoka nje kuwalaki, akawaambia, “Ikiwa mmekuja kwangu kama marafiki ili kunisaidia basi nawapokea kwa moyo wote, lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa maadui zangu, ingawa sijatenda ovu lolote, Mungu wa baba zetu awaone na awakemee.”
18 Hapo Roho akamjia Abishai, mkuu wa hao watu thelathini, naye akasema,“Sisi tu watu wako, ee Daudi,tuko upande wako, ee mwana wa Yese!Amani, amani iwe kwako,na amani iwe kwa yeyote akusaidiaye!Maana akusaidiaye ndiye Mungu wako.”Ndipo Daudi akawapokea na kuwafanya maofisa katika jeshi lake.