17 Daudi akatoka nje kuwalaki, akawaambia, “Ikiwa mmekuja kwangu kama marafiki ili kunisaidia basi nawapokea kwa moyo wote, lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa maadui zangu, ingawa sijatenda ovu lolote, Mungu wa baba zetu awaone na awakemee.”
18 Hapo Roho akamjia Abishai, mkuu wa hao watu thelathini, naye akasema,“Sisi tu watu wako, ee Daudi,tuko upande wako, ee mwana wa Yese!Amani, amani iwe kwako,na amani iwe kwa yeyote akusaidiaye!Maana akusaidiaye ndiye Mungu wako.”Ndipo Daudi akawapokea na kuwafanya maofisa katika jeshi lake.
19 Askari wengine wa kabila la Manase, walitoroka na kujiunga na Daudi, wakati alipoondoka pamoja na Wafilisti kwenda kupigana na mfalme Shauli. (Lakini hata hivyo, hakuwasaidia maana watawala wa Wafilisti walifanya shauri wamfukuze arudi Siklagi wakisema, “Tutayahatarisha maisha yetu kwa sababu atatutoroka arudi kwa bwana wake Shauli.”)
20 Basi, Daudi alipokuwa Siklagi, watu wafuatao wa kabila la Manase walimwendea: Adna, Yozabadi, Yediaeli, Mikaeli, Yozabadi, Elihu na Silethai. Kila mmoja wao alikuwa kiongozi wa kikosi cha watu 1,000 katika kabila la Manase.
21 Walimsaidia Daudi kupigana na magenge ya washambuliaji, kwani wote walikuwa askari mashujaa na makamanda jeshini.
22 Siku hata siku, watu walijiunga na Daudi kumsaidia, hatimaye akawa na jeshi kubwa sana, kama jeshi la Mungu.
23 Hii ndio idadi ya vikosi vya askari wenye silaha waliojiunga na Daudi huko Hebroni ili kumtwalia ufalme kutoka kwa Shauli, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu: