1 Kisha waliliingiza sanduku la Mungu, na kuliweka ndani ya hema ambayo Daudi alikuwa ameitayarisha. Halafu wakatoa tambiko za kuteketezwa na za amani mbele ya Mungu.
2 Daudi alipomaliza kutoa tambiko hizo za kuteketezwa na za amani, aliwabariki watu katika jina la Mwenyezi-Mungu,
3 na akawagawia Waisraeli wote, wanaume kwa wanawake, kila mmoja akapewa mkate, kipande cha nyama na mkate wa zabibu.
4 Zaidi ya hayo, Daudi aliwateua baadhi ya Walawi wawe wahudumu wa sanduku la Mwenyezi-Mungu, wamtukuze, wamtolee shukrani na wamsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.