8 Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza maadui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine wa dunia.
9 Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali,
10 tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli; mimi nitawashinda maadui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba.
11 Siku zako zitakapotimia za kujiunga na babu zako, nitamfanya mmoja wa watoto wako, wewe mwenyewe awe mfalme; nami nitauimarisha ufalme wake.
12 Yeye ndiye atakayenijengea nyumba; nami nitahakikisha kwamba ufalme wake unadumu milele.
13 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; lakini sitamwondolea fadhili zangu kama vile nilivyomwondolea Shauli aliyekutangulia.
14 Bali nitamwimarisha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele, na kiti chake cha enzi kitakuwa imara daima.’”