1 Ikawa baada ya hayo Nahashi, mfalme wa Waamoni akafariki; naye mwanawe akashika utawala.
2 Basi, Daudi akasema, “Nitamtendea mema Hanuni mwana wa Nahashi, kwani baba yake alinitendea mema pia.” Hivyo Daudi alituma wajumbe na kumpelekea salamu za rambirambi kwa ajili ya kifo cha baba yake. Nao wakaenda kwa Hanuni ili kumfariji, huko katika nchi ya Waamoni.
3 Lakini viongozi wa Waamoni wakamwambia mfalme, “Je! Unadhani ni kwa sababu ya heshima ya baba yako ati Daudi ametuma wajumbe hawa waje kukufariji? Watu hawa si majasusi waliotumwa kuja kuichunguza nchi kuiangamiza na kuipeleleza?”
4 Basi Hanuni aliwachukua wajumbe hao wa Daudi, akawanyoa ndevu na kuzipasua nguo zao katikati hadi matakoni, kisha akawatoa waende zao,
5 nao wakaondoka kurudi makwao. Daudi alipopashwa habari jinsi walivyotendewa wajumbe wake, alituma watu kuwalaki kwani hao wajumbe waliona aibu sana. Naye mfalme aliwaambia, “Kaeni mjini Yeriko, hata mtakapoota ndevu, Kisha mrudi.”