19 Daudi akatii amri ya Mwenyezi-Mungu, akapanda juu kufuatana na neno la Gadi alilosema kwa jina la Mwenyezi-Mungu.
20 Ornani alipogeuka na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Ornani alikuwa akipura ngano.
21 Daudi alipomwendea Ornani, Ornani alitazama na kumwona Daudi; basi huyo Ornani alitoka kwenye uwanja wa kupuria akaenda mbele; kisha akamsujudia akiinamisha kichwa chake mpaka chini ardhini.
22 Daudi akamwambia Ornani, “Nipe nafasi ya uwanja wako wa kupuria nafaka ili nimjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu juu yake, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa kwa watu. Niuzie kwa bei yake kamili.”
23 Naye Ornani akamwambia Daudi, “Kichukue kiwanja hiki, bwana wangu mfalme, na ukitumie vile unavyopenda mwenyewe. Tazama, nawatoa fahali kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, na vifaa vya kupuria kwa kuni, pamoja na ngano iwe tambiko ya nafaka. Vyote hivyo ninakupa.”
24 Lakini mfalme Daudi alimwambia Ornani, “La, hasha; nitavinunua kwa thamani yake kamili; sitamchukulia Mwenyezi-Mungu kitu kilicho chako au kumtolea tambiko za kuteketezwa ambazo hazijanigharimu kitu.”
25 Hivyo, Daudi alimlipa Ornani kwa kumpimia shekeli 600 kamili za dhahabu kulipia uwanja huo.