3 Lakini Mungu alinikataza, kwa sababu mimi ni mtu wa vita na nimekwisha mwaga damu nyingi.
4 Lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli alinichagua mimi miongoni mwa jamaa ya baba yangu kuwa mfalme wa Israeli milele. Alilichagua kabila la Yuda liongoze; na kutokana na kabila hilo, aliichagua jamaa ya baba yangu, na miongoni mwa wana wa baba yangu, alipendezwa nami na kuniweka niwe mfalme wa Israeli yote.
5 Mwenyezi-Mungu amenijalia wana wengi, na miongoni mwa hao wote, amemchagua Solomoni mwanangu, aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wake Mwenyezi-Mungu aitawale Israeli.
6 “Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Mwanao Solomoni ndiye atakayenijengea nyumba na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye awe mwanangu, nami nitakuwa baba yake.’
7 Nitauimarisha ufalme wake milele ikiwa ataendelea kuzishika kwa dhati amri na sheria zangu kama anavyofanya leo.
8 “Basi sasa, mbele ya kusanyiko hili la Waisraeli wote, jumuiya ya watu wa Mwenyezi-Mungu, na mbele ya Mungu wetu, angalieni mzishike amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili mwendelee kuimiliki nchi hii nzuri, na kuwarithisha wazawa wenu baada yenu, hata milele.
9 “Nawe Solomoni mwanangu, umjue Mungu wa baba yako, na umtumikie kwa moyo wako wote na kwa nia thabiti; yeye Mwenyezi-Mungu huchunguza mioyo na anafahamu mipango na fikira za binadamu. Ukimtafuta yeye, utamwona; lakini ukimwacha, atakutupilia mbali milele.