7 Nitauimarisha ufalme wake milele ikiwa ataendelea kuzishika kwa dhati amri na sheria zangu kama anavyofanya leo.
8 “Basi sasa, mbele ya kusanyiko hili la Waisraeli wote, jumuiya ya watu wa Mwenyezi-Mungu, na mbele ya Mungu wetu, angalieni mzishike amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili mwendelee kuimiliki nchi hii nzuri, na kuwarithisha wazawa wenu baada yenu, hata milele.
9 “Nawe Solomoni mwanangu, umjue Mungu wa baba yako, na umtumikie kwa moyo wako wote na kwa nia thabiti; yeye Mwenyezi-Mungu huchunguza mioyo na anafahamu mipango na fikira za binadamu. Ukimtafuta yeye, utamwona; lakini ukimwacha, atakutupilia mbali milele.
10 Basi, ujihadhari na kukumbuka ya kwamba, Mwenyezi-Mungu amekuchagua wewe umjengee nyumba ya ibada. Uwe hodari ukatende hivyo.”
11 Ndipo Daudi akampa Solomoni mwanawe ramani ya majengo yote ya hekalu, nyumba zake, hazina zake, ghorofa zake, vyumba vyake vya ndani na mahali pa kiti cha rehema.
12 Alimpa ramani ya yote aliyokusudia moyoni kuhusu nyua za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, vyumba vya Mungu na ghala za kuwekea vitu vilivyo wakfu.
13 Alimpa pia mfano wa jinsi ya kuwapanga makuhani na Walawi kuzitekeleza huduma zao, kutumikia nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuvitunza vyombo vyote vya Nyumba ya Mwenyezi-Mungu.