36 Mimi mtumishi wako nimekwisha ua simba wengi na dubu wengi. Sasa, hata yule Mfilisti asiyetahiriwa, ambaye ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai, atakuwa kama hao.
37 Mwenyezi-Mungu ambaye ameniokoa makuchani mwa simba na dubu, ataniokoa kutoka kwa Mfilisti huyu.” Shauli akamwambia, “Nenda; naye Mwenyezi-Mungu awe pamoja nawe.”
38 Shauli akamvisha Daudi mavazi yake ya kivita, akamvika kofia yake ya shaba kichwani na koti lake la kujikinga kifua.
39 Daudi akajifunga upanga wa Shauli, akajaribu kutembea; lakini akashindwa kwa kuwa hakuyazoea mavazi kama hayo. Akamwambia Shauli, “Siwezi kwenda vitani nikiwa nimevaa mavazi haya, kwani mimi sijayazoea.” Kwa hiyo, akayavua.
40 Daudi akachukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe matano mazuri kutoka kwenye kijito, akayatia katika mfuko wake wa mchungaji. Kombeo lake likiwa tayari mkononi mwake, akaanza kumwendea Goliathi Mfilisti.
41 Yule Mfilisti, naye akaanza kumwendea Daudi, na yule aliyemchukulia ngao yake akiwa mbele yake.
42 Yule Mfilisti alipoangalia na kumwona vizuri Daudi, alimdharau, kwani Daudi alikuwa kijana tu, mwenye afya na wa kupendeza.