1 Daudi alikwenda kwa kuhani Ahimeleki huko Nobu. Ahimeleki akatoka kumlaki huku akiwa anatetemeka, akamwuliza, “Kwa nini umekuja hapa peke yako?”
2 Daudi akamjibu, “Niko hapa kutokana na amri ya mfalme. Aliniambia nisimweleze mtu yeyote juu ya kile ambacho amenituma. Nimeagana na watu wangu kwamba tukutane mahali fulani.
3 Je, una kitu chochote? Nakuomba mikate mitano au chochote kilichoko.”
4 Kuhani Ahimeleki akamwambia, “Hapa sina mkate wa kawaida. Ninayo tu ile mikate mitakatifu. Mnaweza kupewa mikate hiyo ikiwa watu wako hawajalala na wanawake hivi karibuni.”