1 Samueli alipokuwa mzee, aliwafanya watoto wake wa kiume kuwa waamuzi wa Israeli.
2 Mtoto wake wa kwanza wa kiume aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya. Wote wawili walikuwa waamuzi huko Beer-sheba.
3 Lakini watoto hao hawakufuata mwenendo wa baba yao. Bali walianza kujitafutia faida. Wakapokea rushwa na kupotosha haki.
4 Basi, viongozi wote wa Israeli walikusanyika pamoja, na kumwendea Samueli mjini Rama,
5 wakamwambia, “Tazama, wewe sasa ni mzee na watoto wako hawafuati mwenendo wako. Hivyo, tuteulie mfalme wa kututawala kama yalivyo mataifa mengine.”
6 Lakini jambo la Waisraeli kutaka wapewe mfalme wa kuwatawala, halikumpendeza Samueli. Naye akamwomba Mwenyezi-Mungu.
7 Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sikiliza kila kitu ambacho watu wanakuambia; maana hawajakukataa wewe, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme juu yao.