4 Basi, viongozi wote wa Israeli walikusanyika pamoja, na kumwendea Samueli mjini Rama,
5 wakamwambia, “Tazama, wewe sasa ni mzee na watoto wako hawafuati mwenendo wako. Hivyo, tuteulie mfalme wa kututawala kama yalivyo mataifa mengine.”
6 Lakini jambo la Waisraeli kutaka wapewe mfalme wa kuwatawala, halikumpendeza Samueli. Naye akamwomba Mwenyezi-Mungu.
7 Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sikiliza kila kitu ambacho watu wanakuambia; maana hawajakukataa wewe, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme juu yao.
8 Tangu nilipowatoa Misri, wameniacha mimi, wamekuwa wakiitumikia miungu mingine mpaka leo. Sasa hayo matendo ambayo wamekuwa wakinitendea mimi, ndiyo wanayokutendea na wewe.
9 Basi, wasikilize, lakini, waonye vikali, na waeleze waziwazi jinsi mfalme atakayewatawala atakavyowatendea.”
10 Kwa hiyo, Samueli akawaambia wale watu waliokuwa wanaomba wapewe mfalme maneno yote ya Mwenyezi-Mungu.