1 Mfalme Yehoshafati wa Yuda alirejea salama katika ikulu yake mjini Yerusalemu.
2 Lakini mwonaji Yehu mwana wa Hanani, alikwenda kumlaki mfalme, akamwambia, “Je, unadhani ni vema kuwasaidia waovu na kuwapenda wamchukiao Mwenyezi-Mungu? Mambo uliyofanya yamekuletea ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.
3 Walakini, kuna wema fulani ndani yako. Umekwisha ziondoa sanamu zote za Ashera, mungu wa kike, na umejitahidi sana kumtafuta Mungu kwa moyo wote.”
4 Mfalme Yehoshafati alikaa Yerusalemu, lakini hata hivyo, mara kwa mara aliwatembelea watu wa Beer-sheba kusini, mpaka milima ya Efraimu, upande wa kaskazini. Alifanya hivyo ili kuwavutia watu wamrudie Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao.
5 Aliteua waamuzi katika miji yote ya Yuda yenye ngome,
6 akawaambia, “Muwe waangalifu sana wakati mnapoamua, kwa maana hukumu mtoayo hamwitoi kwa amri ya binadamu, bali kwa amri itokayo kwa Mwenyezi-Mungu, naye yu pamoja nanyi mnapotoa uamuzi.