3 Walakini, kuna wema fulani ndani yako. Umekwisha ziondoa sanamu zote za Ashera, mungu wa kike, na umejitahidi sana kumtafuta Mungu kwa moyo wote.”
4 Mfalme Yehoshafati alikaa Yerusalemu, lakini hata hivyo, mara kwa mara aliwatembelea watu wa Beer-sheba kusini, mpaka milima ya Efraimu, upande wa kaskazini. Alifanya hivyo ili kuwavutia watu wamrudie Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao.
5 Aliteua waamuzi katika miji yote ya Yuda yenye ngome,
6 akawaambia, “Muwe waangalifu sana wakati mnapoamua, kwa maana hukumu mtoayo hamwitoi kwa amri ya binadamu, bali kwa amri itokayo kwa Mwenyezi-Mungu, naye yu pamoja nanyi mnapotoa uamuzi.
7 Basi, sasa mwogopeni Mwenyezi-Mungu, muwe waangalifu katika kila jambo mtakalotenda kwa sababu Mwenyezi-Mungu wetu hatavumilia upotoshaji wa haki, wala upendeleo wala ulaji rushwa.”
8 Mjini Yerusalemu, Yehoshafati aliteua Walawi kadhaa, waamuzi na baadhi ya wakuu wa jamaa za Waisraeli wawe waamuzi wa magomvi yahusuyo uvunjaji wa sheria za Mwenyezi-Mungu, au ugomvi baina ya wakazi wa mji.
9 Akawaamuru akisema; “Tekelezeni wajibu wenu mkimwogopa Mwenyezi-Mungu, kwa uaminifu na kwa moyo wote.