4 Tazama, karibu nianze kujenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Nitaiweka wakfu, nayo itakuwa mahali pa kufukiza ubani wa harufu nzuri mbele yake, na mahali pa mikate ya kuwekwa mbele yake daima, na tambiko za kuteketezwa asubuhi na jioni na pia siku za Sabato, mwezi mwandamo, na sikukuu nyinginezo za Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama alivyoiagiza Israeli milele.
5 Nyumba ninayokusudia kujenga itakuwa kubwa sana, kwani Mungu wetu ni mkuu zaidi ya miungu yote.
6 Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba ikiwa mbingu zenyewe hazimtoshi, wala mbingu za juu sana? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba isipokuwa tu kama mahali pa kufukizia ubani mbele yake?
7 Basi, sasa nitumie mtu mwenye ujuzi wa kutengeneza vyombo kwa dhahabu, fedha, shaba, na chuma, na nguo za rangi ya zambarau, za rangi nyekundu na ya samawati, ajuaye pia, kutia nakshi. Yeye atashirikiana katika kazi hiyo na mafundi walioko pamoja nami katika Yuda na Yerusalemu, ambao baba yangu Daudi aliwachagua.
8 Tena nipelekee mierezi, miberoshi na misandali kutoka Lebanoni, kwa maana najua ya kwamba watumishi wako ni hodari sana wa kupasua mbao huko Lebanoni. Nao watumishi wangu watashirikiana na watumishi wako,
9 ili wanipasulie mbao kwa wingi, maana nyumba ninayokusudia kujenga ni kubwa na ya ajabu.
10 Kwa ajili ya watumishi wako, yaani maseremala watakaopasua mbao, nitatoa tani 2,000 za ngano iliyopondwa, tani 2,000 za shayiri, lita 400,000 za divai na lita 400,000 za mafuta.”