5 Hata alifuata shauri lao, akaenda pamoja na mfalme Yehoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu huko Ramoth-gileadi. Nao Washamu walimjeruhi Yoramu.
6 Kisha akarudi Yezreeli ili apate kutibiwa majeraha aliyoyapata huko Rama, wakati alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alimtembelea Yoramu mwana wa Ahabu huko Yezreeli kwa sababu alikuwa mgonjwa.
7 Lakini hiyo ilikuwa imepangwa na Mungu kuwa maangamizi yampate Ahazia kwa njia hiyo ya kumtembelea Yoramu. Maana alipofika huko, alitoka pamoja na Yoramu kwenda kupigana na Yehu mwana wa Nimshi ambaye Mwenyezi-Mungu alimteua kuuangamiza uzao wa Ahabu.
8 Wakati Yehu alipokuwa akiwahukumu jamaa ya Ahabu alikutana na wakuu wa Yuda pamoja na wana wa ndugu zake Ahazia, waliomtumikia Ahazia, akawaua.
9 Alimtafuta Ahazia, naye akakamatwa akiwa amejificha huko Samaria. Walimleta hadi kwa Yehu, akauawa. Waliuzika mwili wake kwani walisema, “Yeye ni mjukuu wa Yehoshafati, ambaye alimtafuta Mwenyezi-Mungu kwa moyo wake wote.”Hapakubaki hata mtu mmoja wa jamaa ya Ahazia ambaye angeweza kuwa falme.
10 Mara Athalia, mamake Ahazia, alipoona kuwa mwanawe ameuawa, alitoka akaangamiza jamii yote ya kifalme ya Yuda.
11 Lakini Yehosheba, binti ya mfalme Yehoramu alimchukua Yoashi, akamtwaa kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Alimficha yeye pamoja na yaya wake, katika chumba cha kulala. Hivyo Yehosheba, binti ya mfalme Yehoramu, mke wa kuhani Yehoadani, kwa sababu alikuwa dadaye Ahazia, alimficha Yoashi ili Athalia asimuue.