15 Alitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu miungu yote ya kigeni na sanamu pamoja na madhabahu zote alizokuwa amezijenga kwenye mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika Yerusalemu; alivitupa nje ya mji.
16 Alirudisha madhabahu ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, na juu yake akatoa tambiko za amani na za shukrani, akawaamuru watu wa Yuda wamwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
17 Hata hivyo watu waliendelea kutoa sadaka mahali pa kufanyia ibada, lakini kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao tu.
18 Matendo mengine ya Manase, sala yake kwa Mungu wake na maneno ya waonaji waliozungumza naye kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hayo, yote yameandikwa katika Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.
19 Nalo ombi lake na jinsi Mungu alivyompokea, dhambi zake zote na ukosefu wa uaminifu wake, mahali alipojenga pa kuabudia na jinsi alivyotengeneza Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekesha, hayo yameandikwa katika Kumbukumbu za Waonaji.
20 Manase alifariki na kuzikwa katika ikulu yake, naye Amoni, mwanawe, akatawala mahali pake.
21 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala Yuda; alitawala miaka miwili huko Yerusalemu.