24 Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili ya mji. Naye mlinzi wa lango akapanda ukutani hadi juu ya lango na alipoinua macho yake aliona mtu anakimbia peke yake.
25 Huyo mlinzi akapaza sauti akamwambia mfalme. Mfalme akasema, “Kama yuko peke yake, lazima ana habari.” Yule mtu akazidi kukaribia.
26 Mlinzi akamwona mtu mwingine anakimbia, akaita tena langoni akisema, “Tazama, mtu mwingine anakimbia peke yake!” Mfalme akasema, “Naye analeta habari.”
27 Yule mlinzi akasema, “Naona kuwa yule anayekimbia zaidi ni Ahimaasi mwana wa Sadoki.” Mfalme akasema, “Huyo ni mtu mwema, anatuletea habari njema.”
28 Ndipo Ahimaasi akamwambia mfalme kwa sauti kubwa, “Mambo yote ni sawa.” Akainama mbele ya mfalme, akasujudu na kusema, “Na atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ambaye amekukomboa kutoka watu walioinua mikono yao dhidi yako, bwana wangu mfalme.”
29 Mfalme akamwambia, “Je, kijana Absalomu hajambo?” Ahimaasi akasema, “Wakati Yoabu aliponituma mimi mtumishi wako, niliona kulikuwa na kelele nyingi, lakini sikufahamu maana yake.”
30 Mfalme akasema, “Kaa kando, na usimame hapo.” Basi, Ahimaasi akaenda kando na kusimama kimya.