15 Watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakaenda kumzingira Sheba akiwa katika mji huo wa Abeli wa Beth-maaka. Walirundika kuuzingira mji, na ngome; halafu wakaanza kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini.
16 Kisha, mwanamke fulani mwenye hekima alisikika kutoka mjini akisema, “Sikieni! Sikieni! Mwambieni Yoabu aje nizungumze naye.”
17 Yoabu akaenda karibu naye, huyo mwanamke akamwambia, “Je, wewe ni Yoabu?” Yoabu akasema, “Naam! Ni mimi.” Yule mwanamke akamwambia, “Nisikilize mimi mtumishi wako.” Yoabu akamwambia, “Nasikiliza.”
18 Huyo mwanamke akamwambia, “Hapo kale watu walikuwa wakisema, ‘Waacheni watake shauri kutoka mji wa Abeli’. Ndivyo watu walivyoweza kutatua matatizo.
19 Mimi ni mmojawapo wa wale wanaopenda amani na uaminifu katika Israeli. Sasa wewe unakusudia kuuharibu mji ambao ni kama mama katika Israeli. Kwa nini sasa unataka kuuangamiza mji ulio mali yake Mwenyezi-Mungu?”
20 Yoabu akamjibu, “Kamwe maishani mwangu! Sina nia kuangamiza wala kuharibu.
21 Ulivyosema si kweli! Lakini mtu mmoja kutoka sehemu ya milima ya Efraimu aitwaye Sheba mwana wa Bikri anataka kumwasi mfalme Daudi. Mtoeni huyo kwangu nami nitaondoka mjini kwenu.” Yule mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake kitarushwa kwako kupitia ukutani.”