13 Mwenyezi-Mungu alituma manabii na waonaji kuionya Israeli na Yuda akisema, “Acheni njia zenu mbaya mkatii amri zangu na maagizo yangu kufuatana na sheria nilizowapa babu zenu, na ambazo niliwapeni kupitia kwa watumishi wangu manabii.”
14 Lakini wao hawakutii; walikuwa wagumu kama babu zao ambao hawakumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.
15 Walikataa kutii maagizo yake; hawakushika agano alilofanya na babu zao; licha ya kupuuza maonyo yake, waliabudu sanamu zisizokuwa na maana mpaka hata wao wenyewe hawakuwa na maana tena; walifuata desturi za mataifa yaliyowazunguka: Walipuuza amri za Mwenyezi-Mungu; wala hawakuzizingatia.
16 Walivunja amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakatengeneza sanamu za miungu ya ndama wawili wa kusubu; vilevile wakatengeneza sanamu za mungu wa kike Ashera wakaabudu na vitu vyote vya angani na wakamtumikia Baali.
17 Waliwatambika watoto wao wa kiume na wa kike kwa miungu ya uongo; wakataka shauri kwa watabiri na wachawi. Walinuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakamkasirisha sana.
18 Basi, Mwenyezi-Mungu akawakasirikia sana watu wa Israeli na kuwafukuza kabisa mbele yake; hakuacha mtu isipokuwa kabila la Yuda peke yake.
19 Lakini hata watu wa Yuda hawakutii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wao; bali walifuata desturi zilizoletwa na watu wa Israeli.