2 Wafalme 14 BHN

Mfalme Amazia wa Yuda

1 Katika mwaka wa pili wa enzi ya Yehoashi mwana wa Yehoahazi huko Israeli, Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala.

2 Alipoanza kutawala alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano, naye alitawala katika Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu.

3 Alitenda yaliyo mema mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwa kama babu yake Daudi. Bali alifanya mambo yote kama Yoashi baba yake;

4 isipokuwa mahali pa ibada milimani hapakuharibiwa na watu waliendelea kutambika na kufukiza ubani mahali hapo.

5 Mara tu Amazia alipojiimarisha mamlakani, aliwaua watumishi waliomuua mfalme, baba yake.

6 Lakini hakuwaua watoto wa wauaji; kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria za Mose, Mwenyezi-Mungu anapotoa amri akisema, “Wazazi hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto hawatauawa kwa ajili ya wazazi wao; bali kila mtu atauawa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”

7 Amazia aliwaua Waedomu 10,000 katika Bonde la Chumvi; aliutwaa kwa nguvu mji wa Sela na kuuita Yoktheeli, na hivi ndivyo unavyoitwa mpaka sasa.

8 Kisha Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi, mwana wa Yehu mfalme wa Israeli akisema, “Njoo tupambane.”

9 Lakini Yehoashi mfalme wa Israeli alimpelekea ujumbe Amazia mfalme wa Israeli, akisema, “Siku moja mbaruti wa Lebanoni uliuambia mwerezi, wa huko Lebanoni pia, ‘Mwoze binti yako kwa mwanangu.’ Lakini mnyama wa mwituni akapita hapo na kuukanyagakanyaga mbaruti huo.

10 Sasa wewe Amazia umewashinda kabisa Waedomu, na moyo wako unakufanya ujivune. Ridhika na utukufu wako, ukakae nyumbani; ya nini kujitafutia taabu zitakazokuangamiza wewe mwenyewe pamoja na watu wako wa Yuda?”

11 Lakini Amazia hakujali. Kwa hiyo Yehoashi mfalme wa Israeli alitoka akakabiliana uso kwa uso na Amazia huko vitani Beth-shemeshi, nchini Yuda.

12 Watu wa Yuda walishindwa na watu wa Israeli na kila mmoja alirudi kwake.

13 Yehoashi mfalme wa Israeli alimteka Amazia mfalme wa Yuda, mwana wa Yehoashi, mwana wa Ahazia huko Beth-shemeshi; halafu akauendea Yerusalemu na kuubomoa ukuta wake kutoka Lango la Efraimu mpaka Lango la Pembeni, umbali wa karibu mita 200.

14 Alichukua dhahabu yote na fedha, hata na vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina ya ikulu; pia alichukua mateka, kisha akarudi Samaria.

15 Matendo mengine yote ya Yehoashi, ushujaa wake na vita alivyopigana na mfalme Amazia wa Yuda yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

16 Yehoashi alifariki, akazikwa katika makaburi ya kifalme huko Samaria. Mwanae, Yeroboamu akatawala mahali pake.

Kifo cha mfalme Amazia wa Yuda

17 Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda aliishi miaka kumi na mitano baada ya mfalme Yehoashi wa Israeli kufariki.

18 Matendo mengine yote ya Amazia yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda.

19 Njama za kumwua Amazia zilifanywa Yerusalemu, kwa hiyo alikimbilia Lakishi, lakini maadui walituma watu wa kumwua huko.

20 Maiti yake ililetwa juu ya farasi na kuzikwa katika makaburi ya kifalme katika Yerusalemu katika mji wa Daudi.

21 Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Azaria akiwa na umri wa miaka kumi na sita, wakamtawaza mahali pa Amazia baba yake.

22 Azaria, baada ya kifo cha baba yake, aliujenga upya mji wa Elathi na kuurudisha kwa Yuda.

Mfalme Yeroboamu wa pili wa Israeli

23 Katika mwaka wa kumi na tano wa enzi ya Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala huko Samaria, akatawala kwa muda wa miaka arubaini na mmoja.

24 Alimwasi Mwenyezi-Mungu akafuata mfano wa mtangulizi wake mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi.

25 Aliikomboa nchi yote iliyokuwa mali ya Israeli, kutoka Pito la Hamathi mpaka Bahari ya Araba. Hivi ndivyo alivyoahidi Mwenyezi-Mungu kwa njia ya mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii, kutoka Gath-heferi.

26 Maana Mwenyezi-Mungu aliona taabu kubwa kwa waliyopata Waisraeli kwani hapakuwa na mtu yeyote wa kuwasaidia.

27 Lakini Mwenyezi-Mungu hakuwa amesema ya kwamba ataangamiza Israeli kabisa, hivyo aliwaokoa kwa njia ya mfalme Yeroboamu mwana wa Yehoashi.

28 Matendo mengine yote ya Yeroboamu, vita alivyopigana kwa ushujaa, na jinsi alivyoikomboa Damasko na Hamathi na kuifanya mali ya Israeli, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

29 Yeroboamu alifariki na kuzikwa katika makaburi ya kifalme na mwanawe Zekaria akatawala mahali pake.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25