1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala Yuda, akatawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka hamsini na mitano.
2 Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kuiga mienendo miovu ya mataifa ambayo yalifukuzwa na Mwenyezi-Mungu wakati watu wake, Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini.
3 Kwa maana alirekebisha mahali pa kuabudia miungu mingine palipoharibiwa na Hezekia baba yake; akajenga madhabahu za kuabudia Baali na kutengeneza sanamu ya Ashera, kama vile alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Isitoshe, Manase aliabudu na kutumikia vitu vyote vya mbinguni.
4 Alijenga madhabahu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema, “Jina langu litaabudiwa katika Yerusalemu.”
5 Katika nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, alijenga madhabahu ya kuabudia sayari.
6 Pia alimtoa mwanawe kuwa sadaka ya kuteketezwa. Alipiga ramli; alibashiri akishirikiana na waaguzi wa mizimu na wachawi. Alitenda maovu mengi mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamkasirisha.
7 Nayo sanamu ya Ashera aliyotengeneza akaiweka katika nyumba ambayo Mwenyezi-Mungu aliizungumzia mbele ya Daudi na mwanawe Solomoni: “Katika nyumba hii na mjini Yerusalemu niliouchagua ndiko mahali nitakapoabudiwa milele.
8 Na iwapo Waisraeli watajali kutenda yote niliyowaamuru na kufuata Sheria zote mtumishi wangu Mose alizowapa, basi sitawaacha wafukuzwe kutoka katika nchi hii ambayo niliwapa babu zao.”
9 Lakini hawakusikia, naye Manase aliwafanya watende dhambi zaidi kuliko zile zilizofanywa na mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyaharibu mbele ya Waisraeli.
10 Ndipo Mwenyezi-Mungu alisema kupitia kwa watumishi wake manabii,
11 “Kwa sababu mfalme amefanya mambo ya kuchukiza, mambo mabaya zaidi ya yale yaliyotendwa na Waamori waliomtangulia, amewafanya watu wa Yuda pia watende dhambi kwa kutumia sanamu zake;
12 basi, sasa, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, tazama nitaleta juu ya Yerusalemu na Yuda, msiba ambao hata yeyote atakayesikia atashtuka.
13 Nitauadhibu Yerusalemu kama vile nilivyofanya Samaria, na mfalme Ahabu na wazawa wake. Nitafuta Yerusalemu kama mtu afutavyo sahani iliyosafishwa na kuiinamisha.
14 Nitawaacha hao watu wa urithi wangu watakaosalia na kuwakabidhi kwa adui zao; watakuwa mawindo na mateka kwa adui zao wote.
15 Nitawatendea hayo yote kwa sababu wameniasi na kunikasirisha tangu wazee wao walipotoka Misri mpaka leo.”
16 Zaidi ya hayo, licha ya dhambi yake alipowakosesha watu wa Yuda wakafanya dhambi kwa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Manase aliwaua watu wengi wasiokuwa na hatia, damu ilijaa toka upande mmoja mpaka upande mwingine wa Yerusalemu.
17 Matendo mengine ya Manase na yote aliyotenda, pamoja na dhambi zake zote, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Yuda.
18 Manase alifariki na kuzikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, katika Bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akatawala mahali pake.
19 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; alitawala miaka miwili huko Yerusalemu. Jina la mama yake ni Meshulemethi, binti Haruzi wa Yothba.
20 Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama vile Manase baba yake alivyofanya.
21 Alifuata njia yote aliyoiendea baba yake na kutumikia sanamu ambazo baba yake alizitumikia na kuziabudu.
22 Alimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zake, hakushika njia ya Mwenyezi-Mungu.
23 Baadaye watumishi wa Amoni walikula njama na kumwua katika ikulu yake.
24 Lakini watu wa Yuda wakawaua wote waliomuua Amoni. Kisha watu hao wa Yuda wakamtawaza Yosia mwanawe mahali pake.
25 Matendo mengine yote ya Amoni yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Yuda.
26 Amoni alizikwa kaburini katika bustani ya Uza; na Yosia mwanawe akatawala mahali pake.