1 Baada ya kifo cha Ahabu, watu wa Moabu waliasi wasitawaliwe na Israeli.
2 Mfalme Ahazia alipokuwa Samaria alianguka kutoka chumba kilichokuwa paani mwa nyumba yake, akaumia vibaya. Kwa hiyo akawatuma wajumbe, akawaambia, “Nendeni kwa Baal-zebubu, mungu wa mji wa Ekroni, mkamwulize kama nitapona ugonjwa huu.”
3 Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia nabii Elia kutoka Tishbe, aende kukutana na wajumbe hao na kuwauliza, “Kwa nini mnakwenda kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli?
4 Mwambieni mfalme kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; hakika utakufa!’”
5 Basi, Elia akawaendea. Wale wajumbe wakarudi kwa mfalme, naye akawauliza, “Mbona mmerudi?”
6 Wakamjibu, “Tumekutana na mtu ambaye alitutuma turudi kukuambia kwamba Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Kwa nini unatuma wajumbe kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Je, hakuna Mungu nchini Israeli? Hutashuka katika kitanda ulichokipanda; bali hakika utakufa!’”
7 Mfalme akauliza, “Ni mtu gani huyo aliyekutana nanyi na kuwaambieni mambo hayo?”
8 Wao wakamjibu, “Alikuwa amevaa vazi la manyoya na mshipi wa ngozi kiunoni.” Mfalme akasema, “Huyo ni Elia kutoka Tishbe!”
9 Hapo mfalme akamtuma kapteni mmoja na watu wake hamsini wamlete Elia. Kapteni huyo akamkuta Elia ameketi mlimani, akamwambia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke.”
10 Elia akamjibu huyo kapteni wa watu hamsini, “Kama mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni na kukuteketeza wewe pamoja na watu wako!” Mara moto ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini.
11 Mfalme akamtuma kapteni mwingine na watu wake hamsini wamlete Elia. Naye akapanda juu akamwambia Elia, “Ewe mtu wa Mungu, mfalme anakuamuru ushuke mara moja!”
12 Elia akamjibu, “Kama kweli mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe pamoja na watu wako!” Papo hapo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza pamoja na watu wake hamsini.
13 Kwa mara nyingine tena, mfalme akatuma kapteni mwingine na watu wake hamsini. Kapteni wa tatu akapanda mlimani, akapiga magoti mbele ya Elia na kumsihi akisema, “Ewe mtu wa Mungu, nakusihi uyathamini maisha yangu, na ya watu wako hawa, usituangamize!
14 Maofisa wawili waliotangulia na watu wao, wameteketezwa na moto ulioshuka kutoka mbinguni; lakini sasa nakuomba uyahurumie maisha yangu.”
15 Hapo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Elia, “Shuka pamoja naye, wala usimwogope.” Basi, Elia akainuka, akashuka pamoja naye mpaka kwa mfalme,
16 akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa sababu ulituma wajumbe kumtaka shauri Baal-zebubu, mungu wa Ekroni – kana kwamba hapakuwa na Mungu katika Israeli ambaye ungemwomba shauri – basi, hutashuka katika kitanda ulichopanda; hakika utakufa.’”
17 Baadaye Ahazia akafariki kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia nabii wake Elia. Na, kwa kuwa Ahazia hakuwa na mtoto wa kiume, Yoramu akawa mfalme mahali pake, katika mwaka wa pili wa utawala wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati, mfalme wa Yuda.
18 Mambo mengine aliyoyatenda mfalme Ahazia, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.