1 Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wanafunzi wa manabii akamwendea Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako, mume wangu amefariki, na kama ujuavyo, alikuwa mcha Mungu, lakini aliyemwia fedha amekuja kuwatwaa wanangu wawili wawe watumwa wake.”
2 Elisha akamwuliza, “Sasa nikusaidieje? Niambie kile ulicho nacho nyumbani.” Mama huyo mjane akamjibu, “Mimi mtumishi wako sina kitu chochote ila chupa ndogo ya mafuta.”
3 Elisha akamwambia, “Nenda kwa jirani zako uazime vyombo vitupu vingi kadiri utakavyopata.
4 Kisha uende, wewe pamoja na wanao, mjifungie ndani ya nyumba, na muanze kujaza mafuta. Kila chombo mnachojaza, kiwekeni kando.”
5 Akaenda na kujifungia ndani ya nyumba na wanawe na kuanza kumimina mafuta ndani ya vyombo.
6 Vilipojaa vyote, akamwambia mwanawe mmojawapo, “Niletee chombo kingine.” Mwanae akamjibu, “Vyote vimejaa!” Hapo mafuta yakakoma kutiririka.
7 Akarudi kwa mtu wa Mungu na kumweleza habari hizo. Naye mtu wa Mungu akamwambia, “Nenda ukauze hayo mafuta na kulipa madeni yako, ndipo wewe na wanao mtaishi kwa kutumia hayo yatakayobaki.”
8 Siku moja Elisha alikwenda Shunemu, ambako alikaa mama mmoja tajiri. Mama huyu akamwalika Elisha kwa chakula, na toka siku hiyo ikawa kawaida Elisha kula chakula kwake kila alipopitia huko.
9 Mama huyo akamwambia mumewe, “Sina shaka kwamba mtu huyu anayefika kwetu kila mara ni mtakatifu wa Mungu.
10 Mbona basi tusimjengee chumba na huko tumwekee kitanda, meza, kiti na taa, ili akitumie kila anapotutembelea?”
11 Siku moja Elisha akaja huko na kuingia chumbani mwake ili apumzike.
12 Akamwuliza mtumishi wake Gehazi, “Mwite huyu mama Mshunami.” Alipomwita alikuja na kusimama mbele yake.
13 Naye Elisha akamwambia Gehazi, “Mwambie, tumeona jinsi alivyotushughulikia; sasa anataka tumtendee jambo gani? Je, angependa aombewe lolote kwa mfalme au kwa jemadari wa jeshi?” Mama Mshunami akamjibu, “Mimi ninaishi miongoni mwa watu wangu.”
14 Elisha akasema, “Tumfanyie nini basi?” Gehazi akamjibu, “Hakika hana mtoto, na mumewe amekuwa mzee.”
15 Elisha akamwambia, “Mwite.” Naye akamwita. Akaja na kusimama mlangoni.
16 Elisha akamwambia “Majira kama haya mwakani, utakapotimia mwaka ujao, wakati kama huu, utakuwa na mtoto mikononi mwako.” Mama akamjibu, “La, Bwana wangu! Wewe ni mtu wa Mungu; usinidanganye mimi mtumishi wako!”
17 Lakini huyo mwanamke akapata mimba na kuzaa mtoto wakati kama huo mwaka uliofuata, kama Elisha alivyokuwa amemwambia.
18 Mtoto huyo alipokua, alitoka siku moja pamoja na baba yake akafuatana na wavunaji,
19 naye akamwambia baba yake, “Ole, kichwa changu! Naumwa na kichwa!” Baba yake akamwambia mtumishi wake mmoja, “Mpeleke kwa mama yake.”
20 Alipofikishwa kwa mama yake, alikaa juu ya magoti ya mama yake mpaka adhuhuri, halafu akafa.
21 Mama yake akampeleka na kumlaza kitandani mwa mtu wa Mungu, akaufunga mlango na kuondoka.
22 Akamwita mumewe na kumwambia, “Nipe mtumishi mmoja na punda mmoja, ili nimwendee mara moja yule mtu wa Mungu, kisha nitarudi.”
23 Mumewe akamwuliza, “Mbona unataka kumwona leo? Leo si siku ya mwezi mwandamo wala Sabato?” Akamjibu, “Usijali.”
24 Akatandika punda na kumwambia mtumishi, “Sasa kaza mwendo, wala usipunguze mpaka nitakapokuambia.”
25 Basi, akaondoka, akaenda mpaka mlima Karmeli alipokuwa mtu wa Mungu.Mtu wa Mungu alipomwona akija, akamwambia Gehazi mtumishi wake, “Tazama, namwona Mshunami akija;
26 kimbia mara moja ukakutane naye na kumwambia, ‘Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo?’” Naye Mshunami akamjibu “Hatujambo.”
27 Alipofika mlimani kwa mtu wa Mungu akamshika miguu, naye Gehazi akakaribia ili amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, “Mwache, kwani ana uchungu mkali, naye Mwenyezi-Mungu hakunijulisha jambo hilo.”
28 Huyo mama akamwambia, “Bwana wangu, je, si nilikuomba mtoto? Kwani sikukusihi usije ukanipa matumaini ambayo yangenipa huzuni baadaye?”
29 Elisha akamwambia Gehazi, “Chukua fimbo yangu, uondoke mara moja. Usisimame njiani kumwamkia mtu yeyote, na mtu yeyote akikuamkia njiani, usipoteze wakati kurudisha salamu. Nenda moja kwa moja mpaka nyumbani na kuweka fimbo yangu juu ya mtoto.”
30 Mwanamke akamwambia Elisha, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na kama wewe uishivyo, sitakuacha.” Basi Elisha akaondoka na kufuatana naye.
31 Gehazi akatangulia mbele, na alipofika akaweka fimbo ya Elisha juu ya uso wa mtoto, lakini hakukuonekana dalili yoyote ya uhai. Akarudi na kukutana na Elisha, akamwambia, “Kijana hakufufuka.”
32 Elisha alipofika, akaingia peke yake chumbani na kuona maiti ya kijana kitandani.
33 Basi, akafunga mlango na kumwomba Mwenyezi-Mungu.
34 Ndipo akajilaza juu ya mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, na macho yake juu ya macho ya mtoto na mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Na alipokuwa amekaa hivyo, mwili wa mtoto ukaanza kupata joto.
35 Elisha akasimama na kutembeatembea chumbani, kisha akarudi na kujilaza tena juu ya mtoto. Mtoto akapiga chafya mara saba, halafu akafungua macho.
36 Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite yule Mshunami.” Alipoitwa Elisha akamwambia, “Mchukue mwanao.”
37 Akainama miguuni pa Elisha kwa shukrani na kumchukua mwanawe.
38 Elisha akarudi Gilgali wakati nchini kulikuwa na njaa. Siku moja, alipokuwa akifundisha wanafunzi wa manabii alimwambia mtumishi wake, “Weka chungu kikubwa motoni, uwapikie manabii.”
39 Mmoja wao akaenda shambani na kuchuma mboga. Huko akaona mtango-mwitu, akachuma matango mengi kadiri alivyoweza kuchukua. Akaja nayo, akayakatakata na kuyatia chunguni bila kuyajua.
40 Chakula kikapakuliwa. Lakini walipokionja wakamlilia Elisha wakisema, “Ee mtu wa Mungu, chakula hiki kitatuua!” Nao hawakuweza kukila.
41 Elisha akaagiza aletewe unga. Akaletewa unga, naye akautia ndani ya chungu na kusema, “Sasa wape chakula wale.” Wakakila, na hapo hakikuwadhuru.
42 Mtu Mmoja akatoka Baal-shalisha, akamletea Elisha mikate ishirini iliyotengenezwa kwa shayiri ya malimbuko ya mavuno ya mwaka huo na masuke mabichi ya ngano guniani. Elisha akamwagiza Gehazi awape watu wale.
43 Mtumishi wake akasema, “Sitawapa kwa sababu hakitawatosha watu 100”. Elisha akasema, “Wape wale, kwa sababu Mwenyezi-Mungu amesema kwamba watakula washibe na kingine kitabaki.”
44 Mtumishi wake akawaandalia chakula, wakala wote wakashiba, na kingine kikabaki, kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.