1 Mfalme Hezekia alipopata habari hizo, alirarua mavazi yake, akavaa gunia akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
2 Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia.
3 Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama ambaye anataka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa.
4 Inawezekana Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya jemadari mkuu, ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakaripia maneno aliyosikia. Kwa hiyo waombee watu waliobaki.’”
5 Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya,
6 aliwaambia “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi, ‘Usiogope kwa sababu ya maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wameyasema kunikebehi.
7 Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi, halafu atarudi katika nchi yake na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’”
8 Kisha yule jemadari mkuu aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akiushambulia mji wa Libna.
9 Halafu mfalme alipopata habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema,
10 “Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda, ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba mji wa Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru.
11 Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, wadhani wewe utaokoka?
12 Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, na Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo babu zangu waliyaangamiza?
13 Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na wa Iva?’”
14 Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, naye akaiweka mbele yake Mwenyezi-Mungu.
15 Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, unayekaa katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa, ni wewe tu uliye Mungu, unayetawala falme zote za ulimwengu. Wewe uliumba nchi na mbingu.
16 Ee Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka kukutukana wewe Mungu uliye hai.
17 Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa na nchi zao.
18 Walitupa miungu yao motoni kwa sababu haikuwa miungu ya kweli, bali sanamu za miti na mawe zilizochongwa na mikono ya watu.
19 Sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, nakusihi utuokoe makuchani mwa Senakeribu, falme zote za dunia zijue kwamba ni wewe peke yako, ee Mwenyezi-Mungu, uliye Mungu.”
20 Kisha Isaya, mwana wa Amozi akatuma ujumbe kwa Hezekia, akisema, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ‘Nimesikia ombi lako kwangu kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru:’
21 Hili ndilo neno la Mwenyezi-Mungu alilosema kumhusu Senakeribu:Anakudharau, anakubeza binti Siyoni,anatikisa kichwa chake nyuma yako binti Yerusalemu.
22 Je, uliyekuwa unamkashifu na kumdhihaki ni nani?Nani umemwinulia sautina kumkodolea macho kwa kiburi?Juu ya Mtakatifu wa Israeli!”
23 Kwa kuwatuma wajumbe wako umemkashifu Bwana,wewe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita,nimekwea vilele vya milimampaka kilele cha Lebanoni.Nimekata mierezi yake mirefu,na misonobari mizurimizuri;nimeingia mpaka ndani yakena ndani ya misitu yake mikubwa.
24 Nimechimba visimana kunywa maji mageninilikausha mito yote ya Misrikwa nyayo za miguu yangu.
25 ‘Je, hujasikia,kwamba nilipanga jambo hili tangu awali?Ninachotekeleza sasa nilikipanga zamani.’Nilikuweka uijenge miji yenye ngomekwa rundo la magofu.
26 Wakazi wake wakiwa wameishiwa nguvu,wametishika na kufadhaika,wamekuwa kama mimea ya shambani,kama majani yasiyo na nguvu.Kama majani yaotayo juu ya paa;yakaukavyo kabla ya kukua.
27 Najua kuketi kwako,na kuamka kwakonako kuingia kwako;nayo mipango yako dhidi yangu.
28 Kwa vile umefanya mipango dhidi yanguna nimeusikia ufidhuli wako,nitatia ndoana yangu puani mwako,na lijamu yangu kinywani mwako.Nitakurudisha njia ileile uliyojia.”
29 Kisha Isaya akamwambia mfalme Hezekia, “Na hii ndio itakuwa ishara kwako Hezekia: Mwaka huu na mwaka ujao mtakula kinachomea chenyewe bila kupandwa. Lakini katika mwaka wa tatu mtapanda na kuvuna mavuno; mtapanda mizabibu na kula matunda yake.
30 Wale watakaobaki katika ukoo wa Yuda wataongezeka na kuwa wengi kama vile mti unavyotoa mizizi yake udongoni na kuzaa matunda juu.
31 Maana kutakuwako watu watakaosalia huko Yerusalemu; naam, huko mlimani Siyoni kutakuwako watu wachache watakaosalimika; maana Mwenyezi-Mungu amedhamiria kukamilisha hayo.
32 “Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya mfalme wa Waashuru: ‘Hataingia katika mji huu wala kuupiga mshale wala kuujia kwa ngao wala kuuzingira.
33 Atarudi kwa njia ileile aliyoijia na wala hataingia katika mji huu,’ ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu.
34 ‘Naam, kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi nitaulinda na kuokoa mji huu.’”
35 Basi, usiku huo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliingia kambini mwa Waashuru na kuwaua watu laki moja. Kulipopambazuka watu wakaamka, hao wote walionekana wakiwa maiti.
36 Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru aliondoka akaenda zake na kukaa Ninewi.
37 Siku moja wakati Senakeribu alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki mungu wake, wanawe wawili, Adrameleki na Sharezeri walimuua kwa upanga, halafu wakakimbilia nchini Ararati. Naye Esar-hadoni, mwanawe akatawala badala yake.