14 Hezekia akatuma ujumbe kwa Senakeribu huko Lakishi na kumwambia, “Nimefanya makosa. Tafadhali, komesha mashambulio yako kwangu; nami nitalipa chochote utakacho.” Mfalme wa Ashuru akaagiza Hezekia amletee tani kumi za fedha na tani moja ya dhahabu.
15 Hezekia akampelekea fedha yote iliyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika hazina za nyumba ya mfalme;
16 kadhalika, alingoa dhahabu kutoka katika milango ya hekalu la Mwenyezi-Mungu na ile dhahabu ambayo yeye mwenyewe aliiweka kwenye mihimili ya mlango; yote akampelekea Senakeribu.
17 Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu, amiri mkuu, mkuu wa matowashi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi kwenda kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Walisafiri na kufika Yerusalemu. Nao walipowasili waliingia na kusimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea Uwanda wa Dobi.
18 Walipomwita mfalme Hezekia walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, ambaye alikuwa msimamizi wa ikulu; Shebna, aliyekuwa katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wa kumbukumbu za mfalme.
19 Ndipo jemadari mkuu alipowaambia, “Mwambieni Hezekia, hivi ndivyo anavyosema mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni ujasiri wa namna gani huu unaouwekea matumaini?
20 Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi?