1 Elisha akamjibu, “Sikiliza neno la Mwenyezi-Mungu: Kesho wakati kama huu, humu Samaria kilo tatu za unga bora wa ngano zitagharimu fedha shekeli moja ya fedha, na kilo sita za shayiri kadhalika zitagharimu fedha shekeli moja.”
2 Kapteni mwaminifu wa mfalme akamwambia Elisha, “Kama Mwenyezi-Mungu mwenyewe angefanya madirisha mbinguni, je, jambo hilo litawezekana!” Elisha akamjibu, “Utaona kwa macho yako mwenyewe, lakini wewe hutakula.”
3 Kulikuwa na watu wanne wenye ugonjwa wa ukoma waliokuwa nje ya milango ya mji wa Samaria ambao walisemezana, wao kwa wao, “Mbona tunakaa hapa tukifa njaa?
4 Hakuna maana ya kuingia mjini kwa sababu huko tutakufa. Kwa hiyo hebu twende kwenye kambi ya Waaramu; inawezekana wakatuua, au wasituue.”
5 Hivyo, giza lilipoanza kuingia, wakaenda kwenye kambi ya Waaramu, lakini walipofika huko, hapakuwa na mtu.
6 Maana Mwenyezi-Mungu alilifanya jeshi la Waaramu lisikie sauti kama ya jeshi kubwa lililokuwa na magari na farasi. Waaramu wakadhani kuwa mfalme wa Israeli amekodisha majeshi ya Wahiti na Wamisri kuja kuwashambulia.
7 Basi, katika usiku huo, Waaramu walikimbia wote ili kuyaokoa maisha yao wakiacha mahema yao, farasi na punda wao, na hata kambi yao jinsi ilivyokuwa.